WEWE NI NANI?
Tunatumia muda mwingi tukijikita katika mambo
ambayo hatuyapendi na yanayotutia hofu. Unapotawaliwa na hofu, woga na
kutokujiamini, taswira ya kwanza utakayokutana nayo unapojaribu kufanya jambo
lolote ni kushindwa. Bila kufahamu kuwa nguvu na muda huo ungewekeza kwenye
kujiamini, ungeweza. Chchote unachokipa nguvu ya fikra hutanuka. Usiufiche uwezo wako wa asili nyuma ya pazia la hofu na
kutojiamini, unajikosesha mafanikio!
Kati ya 34% - 38% ya watu hawafurahii hali
waliyonayo au wanachofanya, hii ni kwa mujibu
wa Psychology Today. Vyanzo vingine
vinakadiria viwango vya juu zaidi. Tafiti zinakisia kuwa watu 8 kati ya 10
hawajiamini kwa kila wanachofanya. Nusu kati ya hao, hukata tamaa kabla hata ya
kujaribu.
Jaribu kufikiria jamii inavyowachukulia watu
wenye mafanikio katika maeneo yako na utagundua kuwa jamii haina mtazamo mzuri
na mafanikio yao.
Tamaduni zetu nyingi zina imani potofu kuhusu Mafanikio na watu waliofanikiwa. Wengi wanachukuliwa kama washirikina au watu wanaofanya vitu vya
hatari kwa siri kufikia mafanikio.
Hutashangaa kusikia, ‘Ooo! Huyu ana pesa za
majini, au yule alitoa kafara mtoto…, mara fulani ni freemason..!’ mradi tu
kuiaminisha jamii kuwa mafanikio siyo kitu rahisi kufikia bila kupitia njia
fulani za ajabu ajabu.
Lakini kabla hujatekwa na mtazamo huu finyu au
kukatishwa tamaa na imani hizi potofu, jaribu kuuchunguza uwezo mkubwa ulio ndani yako. Fahamu kuwa una
nguvu kubwa ndani yako yenye uwezo wa kukupatia chochote unachotaka!
Kama na wewe ni miongoni mwa watu
wengi, wanaoamini kuwa mafanikio huletwa na nguvu fulani kutoka nje, wanaotumia
muda mwingi wakijiambia kuwa hawawezi badala ya kufurahia uwezo wa asili wa
kufanya chochote unachopenda, utakuwa unakosa nafasi ya kufanikisha kile ambacho moyo wako
unakipenda kwa dhati, kwa sababu ya hofu
na kutojiamini. Tafiti hadi tafiti zinaonyesha
kuwa watu ambao huamini kuwa wanaweza, huweza!
PANGA USHINDI KAMA SHUJAA.
Watu wanaofanikiwa katika mambo mbalimbali
hutawaliwa na fikra za ushindi
wanapofanya kile wanachokitaka lakini wanaoshindwa mara kwa mara ni wale
wanaotawaliwa na hofu. Kwa nini usiwe upande wa watu wanaofanikiwa
KUWA MAKINI NA UNACHOKITAKA
Kama hauna furaha na hali
uliyonayo sasa, hakuna uwezekano wa kuwa na furaha hata kama utapata
unachotamani kupata.
Mwanamke mmoja alitamani kuolewa
ili akamilishe furaha yake, lakini alipofanikiwa
kuolewa aligundua kuwa furaha yake bado haijakamilika kwa kuwa mume wake hakuwa
na pesa za kutosha.
Ukweli ni kwamba furaha huanzia
moyoni.Furaha haitegemei kltu. Furaha
ndiyo chemchem ya vitu vyote unavyohitaji maishani.
Ili uweze kufanikisha chochote
unachohitaji maishani fuata kanuni hii;
1. Kwanza
kuwa na furaha, utulivu wa akili/nafsi na amani moyoni. (Kuwa unavyotaka kuwa)
2. Pili,
Fanya unachotaka kufanya
3. Utafanikisha
unachotaka.
Hii ndiyo kanuni wanayoifuata watu
waliofanikiwa duniani.
Lakini watu wengi tunaishi kinyume
na ndiyo maana mafanikio kwetu yanakuwa ni ndoto.
1. Tunataka
kuwa na vitu tunavovitaka (pesa, gari, nyumba, umaarufu nk.)
2. Ili
tufanye zaidi tunachotaka
3. Tuweze
kuwa na furaha
Hii ndiyo sababu inayowafanya watu
wausake utajiri kwa hali na mali (ikiwemo imani potofu) wakiamini kuwa
wakiupata utajiri watakuwa na furaha. Matokeo yake badala ya furaha huandamwa
na matatizo kibao.
Utajiri ni matokeo ya furaha
uliyonayo. Furaha siyo matokeo ya utajiri ulionao.
WEWE NI NANI ?
Ninaamini kuwa kila mtu
aliletwa humu duniani kwa lengo maalumu. Kila
mtu ana kitu ambacho ni cha pekee kinaweza kuchangia maendeleo ya dunia
tunayoishi. Kuweza kukigundua na kukifanyia kazi kitu hicho ili kilete matunda
kwako na kwa wengine ni sawa na kupanda mbegu njema katika dunia hii kwa vizazi
vijavyo.Kwangu mimi, hii ndiyo inabeba maana nzima ya neno MAFANIKIO.
Kuna usemi usemao ‘Mtu anayeishi
bila lengo anapoteza sifa ya kuitwa mtu. Ni sawa meli au ndege inayosafiri bila rada.’
Ukishaamua kufanya jambo
ambalo unaamini kwa moyo wako wote kuwa
ndilo lengo kuu katika maisha yako na
ukajipa imani kuwa umezaliwa kufanya unachotaka kufanya, hakuna kitakachokuzuia
kufikia mafanikio.
Vitu vifuatavyo vitakuongoza:
1. Shauku/Usongo
wa kitu/jambo unalotaka kufanya au unavyotaka kuwa. Jiulize mwenyewe, je, unakipenda kwa dhati unachotaka kufanya? unakifurahia? kipo damuni/ moyoni? una nia nacho?
unakihitaji?
2. Imani.
Jiamini wewe na lengo unalotaka kulifanikisha. Amini kwamba una uwezo na kila
sababu ya kushinda. Kujiamini ni ushindi kabla ya vita. Ni kujiweka karibu
kabisa na malengo yako.
3. Jikubali.
Kuwa tayari kupokea matokeo yoyote yanayotokana na mchakato mzima wa
ufanikishaji wa malengo yako. Jirekebishe haraka unapohisi umekosea na uwe
tayari kubeba majukumu yote ya mchakato mzima.

Kaka umwongea kweli. Asante kwa kunifumbua macho
JibuFuta