Jumatano, 17 Desemba 2014

UMEJIANDAAJE KISAIKOLOJIA KUFIKIA MALENGO YAKO?



 Washauri wa maendeleo binafsi  (Self Development)  wanatuambia  kwamba mikakati (strategies) huchangia asilimia 20 tu ya mafanikio ya mtu. Asilimia 80 hutokana na maandalizi ya kisaikolojia.

Hii ina maana kwamba maandalizi bora ya kisaikolojia ndiyo huchukua nafasi kubwa katika kufanikisha malengo yako.
Lakini wengi wetu tunakwenda kinyume. Tunapanga mikakati 100% na kusahau kabisa suala la saikolojia na wengine hatuna kabisa habari na kitu hiki. 
Tunafikiri kwamba tukiwa na mikakati mizuri tu tutafanikiwa.

Mikakati inaposhindwa kukufikisha kwenye malengo, unaanza lawama; “sina bahati… nimehujumiwa…serikali yetu haina sapoti…” tunalaumu ndugu na jamaa, tunalaumu wafanyakazi wenzetu, tunalaumu ndugu na jamaa na marafiki.

Hatutaki kuwajibika na matokeo yetu. Badala ya kukubali mapungufu yetu, kuzipokea changamoto na kuzifanyia kazi,  tunatafuta mchawi wa kumbebesha mzigo wa lawama.
Na kisha tunajiridisha kwa kuwachukulia wale waliofanikiwa kuwa hawakutumia njia halali. Wamehonga, wametoa rushwa, washirikina, mafreemason nk. 

Kuanguka au kufanikiwa kwa mtu huanzia kwenye fikra zake. 

Haijalishi askari ana mbinu kali au silaha bora kiasi gani, akiingia vitani na fikra za kushindwa, atashindwa tu.

Fikra ndio kila kitu. Weka fikra chanya kwenye malengo yako utaona mikakati inafanya kazi. Weka fikra hasi, utaona mikakati inakwama.

Mikakati ni nyenzo tu za kukuwezesha kuyafikia malengo yako. Nyezo pekee yake haziwezi kukufikisha unakotaka kwenda kama haukotayari au hujajiandaa kisaikolojia.

 Fikiria kuwa unataka kwenda ghorofa ya kumi na ngazi ndiyo nyenzo pekee ya kukufikisha, bila kujiandaa kisaikolojia utapataje msukumo na nguvu ya kupanda hizo ngazi?

Kuna maandalizi mengi ya kisaikolojia, hapa nitagusia baadhi tu.

       Uchu/shauku. Moyo wako ukitawaliwa na shauku kali ya kufanikisha malengo yako utakuwa na nguvu na msukumo wa kimwili na kiakili wa kuitumia  mikakati yako kukufikisha kwenye malengo yako.

Bila kuwa na uchu/shauku kubwa ni rahisi kukata tamaa na kuvunjika moyo endapo utakutana na vikwazo hata kama ni vidgo tu. Hutakuwa na moyo wa kupambana.

      Kujiamini. Jiamini wewe mwenyewe kuwa unaweza na kile unachokitaka kuwa kinawezekana. Unapojiamini unakuwa na nguvu na unajiweka karibu na malengo yako.
Unapokuwa na hofu unakuwa dhaifu na unajiweka mbali na malengo yako. Kujiamini ni kuwa na mtazamo chanya wa kufanikiwa kwa kile unachokifanya.

      Imani.  Ondoa imani zote potofu juu ya kile unachokitaka. Unapokuwa na imani zinazokinzana baina ya fikra na malengo,  si rahisi kufanikiwa. Kwa mfano, watu wengi tuna imani potofu kuhusu pesa ilihali tunazitaka kwa hali na mali. Methali hizi kuhusu pesa zinakinzana;  pesa asali ya roho/pesa chanzo cha matatizo.
Watu wengi tunaamini kuwa pesa hupatikana kwa kazi ngumu.  Imani hujenga. Ukiamini kuwa pesa ni ngumu basi itaendelea kuwa ngumu. Ukiamini kuwa pesa ni rahisi itakuwa rahisi tu. Ni imani tu. Ukiamini unaweza, utaweza. Ukiamini huwezi hutoweza kamwe.

Kwa ujumla, bila kuwa na maandalizi mazuri ya kisaikolojia, mikakati pekee haitasaidia kukufikisha unakotaka. Ni muhimu kuwa na mikakati mizuri na maandalizi mazuri ya kisaikolojia tunapopanga kufanikisha malengo yetu.


Mungu akubariki.

0 comments:

Chapisha Maoni