Jumapili, 14 Desemba 2014

Mwongozo Wa Mafanikio.

WEWE NI NANI?

Tunatumia muda mwingi tukijikita katika mambo ambayo hatuyapendi na yanayotutia hofu. Unapotawaliwa na hofu, woga na kutokujiamini, taswira ya kwanza utakayokutana nayo unapojaribu kufanya jambo lolote ni kushindwa. Bila kufahamu kuwa nguvu na muda huo ungewekeza kwenye kujiamini, ungeweza. Chchote unachokipa nguvu ya fikra hutanuka. Usiufiche uwezo wako wa asili nyuma ya pazia la hofu na kutojiamini, unajikosesha mafanikio!

Kati ya 34% - 38% ya watu hawafurahii hali waliyonayo  au wanachofanya, hii ni kwa mujibu wa Psychology Today. Vyanzo vingine vinakadiria viwango vya juu zaidi. Tafiti zinakisia kuwa watu 8 kati ya 10 hawajiamini kwa kila wanachofanya. Nusu kati ya hao, hukata tamaa kabla hata ya kujaribu.

Jaribu kufikiria jamii inavyowachukulia watu wenye mafanikio katika maeneo yako na utagundua kuwa jamii haina mtazamo mzuri na mafanikio yao.

Tamaduni zetu nyingi zina imani potofu kuhusu Mafanikio na watu waliofanikiwa. Wengi wanachukuliwa kama washirikina au watu wanaofanya vitu vya hatari kwa siri kufikia mafanikio.

Hutashangaa kusikia, ‘Ooo! Huyu ana pesa za majini, au yule alitoa kafara mtoto…, mara fulani ni freemason..!’ mradi tu kuiaminisha jamii kuwa mafanikio siyo kitu rahisi kufikia bila kupitia njia fulani za ajabu ajabu.

Lakini kabla hujatekwa na mtazamo huu finyu au kukatishwa tamaa na imani hizi potofu, jaribu kuuchunguza  uwezo mkubwa ulio ndani yako. Fahamu kuwa una nguvu kubwa ndani yako yenye uwezo wa kukupatia chochote unachotaka!

Kama na wewe ni miongoni mwa watu wengi, wanaoamini kuwa mafanikio huletwa na nguvu fulani kutoka nje, wanaotumia muda mwingi wakijiambia kuwa hawawezi badala ya kufurahia uwezo wa asili wa kufanya chochote unachopenda, utakuwa unakosa  nafasi ya kufanikisha kile ambacho moyo wako unakipenda kwa dhati,  kwa sababu ya hofu na kutojiamini.  Tafiti hadi tafiti zinaonyesha kuwa watu ambao huamini kuwa wanaweza, huweza!

PANGA USHINDI KAMA SHUJAA.


Watu  wanaofanikiwa katika mambo mbalimbali hutawaliwa na fikra za ushindi  wanapofanya kile wanachokitaka lakini wanaoshindwa mara kwa mara ni wale wanaotawaliwa na hofu. Kwa nini usiwe upande wa watu wanaofanikiwa

KUWA MAKINI NA UNACHOKITAKA


Kama hauna furaha na hali uliyonayo sasa, hakuna uwezekano wa kuwa na furaha hata kama utapata unachotamani kupata.

Mwanamke mmoja alitamani kuolewa ili akamilishe furaha yake, lakini  alipofanikiwa kuolewa aligundua kuwa furaha yake bado haijakamilika kwa kuwa mume wake hakuwa na pesa za kutosha.

Ukweli ni kwamba furaha huanzia moyoni.Furaha haitegemei kltu.  Furaha ndiyo chemchem ya vitu vyote unavyohitaji maishani.

Ili uweze kufanikisha chochote unachohitaji maishani fuata kanuni hii;

1.  Kwanza kuwa na furaha, utulivu wa akili/nafsi na amani moyoni. (Kuwa unavyotaka kuwa)

2.  Pili, Fanya unachotaka kufanya

3.  Utafanikisha unachotaka.

Hii ndiyo kanuni wanayoifuata watu waliofanikiwa duniani.

Lakini watu wengi tunaishi kinyume na ndiyo maana mafanikio kwetu yanakuwa ni ndoto.

1.  Tunataka kuwa na vitu tunavovitaka (pesa, gari,      nyumba, umaarufu nk.)

2.  Ili tufanye zaidi tunachotaka

3.  Tuweze kuwa na furaha

Hii ndiyo sababu inayowafanya watu wausake utajiri kwa hali na mali (ikiwemo imani potofu) wakiamini kuwa wakiupata utajiri watakuwa na furaha. Matokeo yake badala ya furaha huandamwa na matatizo kibao.

Utajiri ni matokeo ya furaha uliyonayo. Furaha siyo matokeo ya utajiri ulionao.

WEWE NI NANI ?

Ninaamini kuwa kila mtu aliletwa  humu duniani kwa lengo maalumu. Kila mtu ana kitu ambacho ni cha pekee kinaweza kuchangia maendeleo ya dunia tunayoishi. Kuweza kukigundua na kukifanyia kazi kitu hicho ili kilete matunda kwako na kwa wengine ni sawa na kupanda mbegu njema katika dunia hii kwa vizazi vijavyo.Kwangu mimi, hii ndiyo inabeba maana nzima ya neno MAFANIKIO.

Kuna usemi usemao ‘Mtu anayeishi bila lengo anapoteza sifa ya kuitwa mtu. Ni sawa meli au ndege inayosafiri bila rada.’

Ukishaamua kufanya jambo ambalo  unaamini kwa moyo wako wote kuwa ndilo lengo kuu  katika maisha yako na ukajipa imani kuwa umezaliwa kufanya unachotaka kufanya, hakuna kitakachokuzuia kufikia mafanikio.

Vitu vifuatavyo vitakuongoza:

1.  Shauku/Usongo wa kitu/jambo unalotaka kufanya au unavyotaka kuwa.  Jiulize mwenyewe, je, unakipenda  kwa dhati unachotaka kufanya? unakifurahia? kipo damuni/ moyoni? una nia nacho? unakihitaji?

2.  Imani. Jiamini wewe na lengo unalotaka kulifanikisha. Amini kwamba una uwezo na kila sababu ya kushinda. Kujiamini ni ushindi kabla ya vita. Ni kujiweka karibu kabisa na malengo yako.

3.  Jikubali. Kuwa tayari kupokea matokeo yoyote yanayotokana na mchakato mzima wa ufanikishaji wa malengo yako. Jirekebishe haraka unapohisi umekosea na uwe tayari kubeba majukumu yote ya mchakato mzima.

Maoni 1 :