Alhamisi, 18 Desemba 2014

HATUA 10 ZA KUFANIKISHA MALENGO YAKO 2015.


Safari ya kufikia Mafanikio, katika malengo yoyote uliyojiwekea inaweza kuchukua muda mrefu au mfupi kulingana na ulivyojipanga na hatua unaochukua. 

Hatua zifuatazo zitakusaidia kufanikisha malengo utakayojiwekea kwa mwaka ujao wa 2015 kwa haraka zaidi.

1.UFASAHA WA LENGO


Ni lazima ufahamu matokeo ya kile unachotaka kufanya, nikimaanisha kuwa ni lazima uwe na picha halisi ya kile unachotaka kukifanikisha. Lazima ujue unataka nini au unataka kuwa nani.
Lengo lazima liwe wazi, lijulikane kabla hujaanza kuchukua hatua yoyote. Kwa maana nyingine huwezi kuanzisha safari pasipo kujua mwisho wa safari yako.
Unapokuwa na lengo mahususi ni rahisi kupanga mikakati ya kulifanikisha. Akili na mawazo huanza kuvutia vitu ambavyo vitarahisisha ufanikishaji wa lengo lako. Ni vema kujikita hasa kwa kile unachohitaji na kuachana na yale usiyoyahitaji. Kuielekeza akili yako kwenye mambo usiyoyataka utavutia fikra hasi na kukosa hamasa na msukumo wa kuchukua hatua zaidi za kuelekea kwenye malengo yako.

2. CHUKUA UAMUzI  THABITI

Baada ya kugundua lengo mahususi ni wakati wa kuchukua uamuzi mathubuti wa kufikia Malengo yako. Ni wakati wa kuamua kuwa unaenda kufanya kile unachotaka kufanya kwa moyo wako wote, nguvu zako zote na akili yako yote na kwamba ni lazima ufanikiwe kwa vyovyote vile. Uamuzi huu lazima uwe umetoka moyoni mwako na si shinikizo au ushawishi wa watu wengine.
Uamuzi thabiti unadhihirisha kuwa kitu ulichoamua kufanya unakipenda na kimo katika damu yako. Kwa kufanya kitu ambacho ni shauku ya moyo wako ni rahisi kwako kuzigeuza changamoto utakazokutana nazo  kuwa fursa zitakazokurahisishia safari ya kuyafikia Malengo yako. Hautoweza kukata tamaa kwa urahisi hata pale mambo yanapoonyesha kuwa magumu.

3.CHUKUA WAJIBU BINAFSI

Tambua kwamba uamuzi uliouchukua ni wako binafsi kwa hiyo uwe tayari kuyapokea mambo yote ya sasa na yajayo yatakayotokana na uamuzi uliouchukua. Upo tayari kubeba lawama au pongezi. Hakuna mtu ambaye utamlaumu kwa lolote litakalotokea, hakuna wa kumsingizia wala kumyooshea kidole. Changamoto zote utazitatua mwenyewe na utakapoanguka utasimama mwenyewe. Kwa maana nyingine, usitegemee sana msaada watu wengine.

4. JIAMINI

Kujiamini kunakuweka karibu na Malengo yako. Woga unakuweka mbali na Malengo yako. Kujiamini ni nyenzo kubwa katika kufanikisha Malengo yako. Kujiamini ni kushinda  vita kabla ya pambano. Jiamini na unachokifanya na utazipenda hatua zote unazochukua kuyafikia Malengo yako.

5. UNGANA KIHISIA NA KILE UNACHOTAKA KUFANIKISHA.

Vuta picha mbalimbali za kihisia kwa lengo unalotaka kulifanikisha na ujione kana kwamba tayari umeshafanikiwa. Kama hamu yako ni kuwa daktari jione kwamba umeshakuwa daktari jione kuwa uko katika chumba cha daktari unawahudumia wagonjwa wako kwa furaha na wao wanafurahia huduma yako. Kama unapenda kuwa mfanyabiashara mkubwa vuta picha kihisia ukijiona upo na wateja unawahudumia au una saini hundi ama unaadaa manunuzi ya bidhaa. Kwa kufanya hivi unaihadaa akili yako fichika (subconscious mind) ambayo haijui kutofautisha kati ya jambo halisi na lisilohalisi hivyo itakuweka katika mazingira yanayoendana na picha unayoijenga akilini na kuvutia mambo ambayo yatakurahisishia kufanikisha malengo yako.

6.TAMBUA CHA KUFANYA KUKUFIKISHA KATIKA MALENGO YAKO

Lazima ujuwe ni nini cha kufanya kukufikisha katika malengo yako. Kwa lugha nyingine ni hatua gani uchukue ili kufikia malengo yako.

7. JIWEKEE MPANGO KAzI

Mpango kazi unahusisha kulivunja lengo kuu katika malengo madogomadogo ili kuweka urahisi wa kufanikisha adhma yako. Hii ni pamoja na kujipangia muda maalumu wa kufanikisha lengo lako, na kupanga mikakati itakayokusaidia.  Bila kuwa na mpango kazi uliojiandalia wewe mwenyewe unajipunguzia uwezekano wa kuyafikia malengo yako kwa muda na wakati unaotakiwa. Pia kuna uwezekano wa kuhama kabisa kwenye lengo na kujikuta unaelekea kwenye lengo jingine kabisa ambalo hukulitegemea. Zaidi ya hayo, unapojiandalia mpango kazi unajipa hamasa binafsi ya kuwekeza akili, mawazo na nguvu zaidi katika malengo yako.
Ni muhimu kuwa na mpango kazi zaidi ya mmoja  yenye mikakati tofauti ili usipoteze mwelekeo pale mpango mkuu unapofeli. (mfano Plan A, Plan B, Plan C, nk).

8. CHUKUA HATUA

Baada ya kujua nini cha kufanya, na kujiandalia mpango kazi, anza mara moja kuchukua hatua, hakuna haja ya kusubiri kila kitu kiwe tayari. Kumbuka, safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Anza na ulichonacho hata kama hakijatimia na utaona hatua nyingine zinajiongeza zenyewe. Utaanza kuona njia inafunguka na kukuonyesha mwelekeo. Chukua hatua sasa! Bila kuchukua hatua yoyote itakuwa vigumu kufikia Malengo yako. Kumbuka kuwa pamoja na kuwa na mipango, mikakati na malengo mazuri, bila kuchukua hatua madhubuti hakuna kitakachoemdelea.

9.JITATHMINI

Je, hatua ulizochukua zinakupeleka karibu na Malengo yako au nje ya Malengo. Kama hatua unazochukua zinakuelekeza katika kufanikisha Malengo yako, basi endelea kuchukua na kuboresha hatua hizo. Lakini kama hatua unazochukua zinakupeleka nje ya Malengo yako jibu siyo kubadili Malengo……
Jibu ni……..

10. BADILI MIKAKATI

Badili mikakati na hatua unazochukua kuelekea katika malengo yako.
Na kama bado haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Badili mikakati na hatua unazochukua.
Na kama bado haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Tumia Plan B.
Na kama bado haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Tumia Plan C.
Na kama bado haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Endelea kubadili mikakati yako, Mpaka utakapofanikiwa.
Hakuna kukata tamaa, hakuna kurudi nyuma.

Kila la kheri. 

0 comments:

Chapisha Maoni