Unapowasikiliza
watu waliofanikiwa kutimiza malengo yao kitu kikubwa wanachojivunia ni namna
walivyozipokea na kuzifanyia kazi changamoto walizokutana nazo.
Watu hawa
huzipokea changamoto kama baraka, wakiamini kuwa nyuma ya changamoto hizi zimejificha fursa kubwa zinazopelekea ufumbuzi
wa jambo wanalolishughulikia.
Hakuna fursa
inayojitokeza waziwazi. Fursa huja zikiwa zimejificha nyuma ya changamoto.
Utayari wako na moyo wa ujasiri wa kupambana na changamoto hizo ndiyo kutawezesha
kuibua fursa nyingi zitakazo kuletea mafanikio.
Watu wengi
tunashindwa kufikia mafanikio ya kweli kwa sababu tunazipokea changamoto kwa mtazamo hasi.
Tunazipokea changamoto kama mikosi, laana au balaa fulani.
Tumesikia
watu wengi wakijinyonga baada ya kufeli mitihani, wengine wakijiua baada ya
kufukuzwa kazi, wengine wakinywa sumu baada ya kuachwa na wapenzi wao, na wengine wakikata tamaa kabisa baada
ya kufilisika kibiashara.
Pengine
kulikuwa na fursa kubwa nyuma ya changamoto hizo endapo watu hawa wangejipa
ujasiri kidogo na kuzikabili changamoto hizo kwa mtazamo chanya. Nani anajua?
Kuna usemi
maarufu usemao kuwa “changamoto zipo kwa ajili ya binadamu”. Ninavyoamini kila
changamoto huwa na sababu ndani yake.
Maendeleo yoyote unayoyaona leo duniani
yametokana na changamoto zilizoshughulikiwa na watu. Kama kila mtu angekuwa anakimbia
changamoto anazokutana nazo naamini kusingekuwa na maendeleo yoyote duniani.
Tusingekuwa
na viongozi wakubwa duniani kama wasingekutana na changamoto kubwa. Alexander
The Great, Napoleon, Mandela, Nyerere, taja na wengine unaowajua,wanajulikana
na kuheshimika sana duniani kwa ujasiri wao wa kuzikabili changamoto
walizokutana nazo.
Watu maarufu na matajiri wakubwa duniani wote walikutana na joto la changamoto kibao kabla hawajaanza kufurahia matunda ya uvumilivu wao.
Niliwahi kusikia kuwa Thomas Edson alifanya zaidi ya majaribio elfu moja kabla hajagundua taa ya umeme (light bulb). Angekata tamaa pengine tungekuwa bado gizani.
Ukimwangalia Oprah Winfrey leo huwezi kufikiri kuwa alizaliwa na kulelewa na mama yake tu, katika mazingira duni ya kijijini huko Mississippi Marekani, au aliwahi kuzaa akiwa na miaka 14 tu (bahati mbaya mtoto alifariki akiwa bado mchanga).
Akiwa mtoto Oprah alivaa nguo zilizotengenezwa kwa magunia ya viazi, ndivyo ambavyo familia yake ilimudu. Lakini leo je? Oprah ni mwanamke mwenye ushawishi mkubwa Duniani, akimiliki media empire, jina kumbwa na utajiri mkubwa. Huwezi kumkuta tena amevaa magunia ya viazi, labda kama itakuwa ni sehemu ya fasheni!
Steve Wonder alizaliwa kipofu, lakini hiyo haikumzuia kuwa mwanamuziki mwenye mafanikio makubwa nchini Marekani, akishinda grammy awards 22 ndani ya miaka 51 aliyoitumikia katika muziki.
umewahi kumsikia Legson Kayira? Ni Professor Maarufu wa Cambrige University. Alizaliwa Malawi katika jamii masikini kupindukia. Alitembea kwa miguu umbali wa zaidi ya maili 3000 kutoka Malawi hadi Cairo Misri kutafuta usafiri (meli) wa kuelekea Marekani akiwa hana hata senti, Baada ya kusoma na kuhamasishwa na kitabu cha historia ya Abraham Lincoln. Kutokana na moyo wa kijasiri alifanikiwa kupambana na changamoto nyingi hadi kufika Marekani na kupata elimu aliyoitaka. yaliyofuata ni historia!!!
Pamoja na changamoto nyingi za enzi za ubaguzi wa rangi nchini afrika kusini, Nelson Mandela alifanikiwa kusoma sheria japo ilikuwa ngumu sana chini ya mfumo huu wa kibaguzi kwa Mwafrika kusomea mambo ya sheria. Mandela aliitumia taaluma yake ya sheria kuwatetea waafrika wenzake katika mfumo wa kibaguzi. Mandela alifungwa kwa kosa lakuupinga mfumo wa kibaguzi miaka ya 1960 .Baada yakutoka gerezani alikofungwa kwa miaka 27 Mandela alifanikiwa kuukomesha mfumo huu wa kibaguzi na kuleta utawala wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini.
Wapo wengi sana waliopitia changamoto kubwa kama hizi ambazo baadae zilizaa neema na kuwanufaisha watu. Watu hawa hawakuwa na tofauti na mimi au wewe zaidi ya ujasiri na kutokata tamaa.
Bila changamoto hakuna Mafanikio.
Jibu ni kupambana tu. Kwani, hata wewe unaweza!
.jpg)
0 comments:
Chapisha Maoni