Jumapili, 14 Desemba 2014

MAFANIKIO NI KUTIMIZA NDOTO.

MAFANIKIO NI KUTIMIZA NDOTO.

Kila mtu ana ndoto fulani ambayo angependa kuiona siku moja inatimia na kuwa kweli.

Swali la kujiuliza ni kwamba, je, unaitambua ndoto yako?unaifanyia kazi ndoto yako? Kama hujafanya juhudi yoyote ya kuitambua na kuifanyia kazi ndoto yako, watu wengine watakutumia ili kutimiza ndoto zao.

Kwa kila  tunachofanya, aidha tunafanya kwa ajili ya kutimiza malengo yetu ama tunawatumikia wengine kutimiza malengo yao.

Ndoto yako ndiyo itakayobainisha malengo yako maishani.

Ndoto ni wazo lolote lililo kichwani mwako ambalo bado halijajidhihirisha katika ulimwengu halisi.

 Kichwani kwako unaweza ukawa na kitabu kizuri ambacho bado hakijaandikwa, wimbo mzuri ambao bado haujaimbwa, daktari au mwanasheria mzuri ambaye bado hajahitimu, biashara ambayo haijaanzishwa, ugunduzi ambao haujawekwa hadharani, mchezaji mzuri ambaye bado hajaonekana na vitu vingine kama hivyo. Hizi zote ni ndoto zinazotafuta nafasi katika ulimwengu halisia.

Unapoingundua ndoto yako na kuifanya kuwa lengo lako maishani, maisha huwa marahisi na yenye furaha. Kazi inakuwa ni sehemu ya maisha badala ya kitu unachofanya ili uishi. Kila kitu unachofanya kinakuwa ni kitu cha kukupatia furaha na kukamilisha malengo yako.

Siyo kwamba unapofuata ndoto yako ndiyo kila kitu kitakuwa rahisi, hapana. Utakutana na mambo mengi tu ya kukuvunja moyo na kukatisha tamaa. Unachotakiwa ni kujipa moyo na kusonga mbele.

Ndoto yako inaweza kuchukua muda mrefu au mfupi kutimia kulingana na hatua unazochukua na jinsi unavyozishughulikia changamoto zinazojitokeza.

Unaweza ukawa na visingizio vingi na sababu za kutosha kuelezea kwa nini maisha yako hayawi kama unavyotaka , lakini hutoweza kuwa na furaha wala kufikia mafanikio ya kweli kama hutaitambua na kuifuata ndoto yako kuu.
Wewe ndiye mwenye usukani wa maisha yako. Unataka kuwa nani, unataka uishi vipi, ufanye nini, ufanikishe kipi,  ni maamuzi yako mwenyewe na si ya mtu mwingine.

Neno la Tahadhari:

Unapoamua kuchukua uamuzi wa kuifuata ndoto yako na kutimiza malengo yako, watu wengi watakukatisha tama, watakuvuta chini, watainanga ndoto yako na kuyapuuza mawazo yako.

 Watasema kuwa uachokifikiria hakifai na kakiwezekani. Watadai kuwa huna uwezo wa kufanya unachotaka kufanya.

Unapowaambia wengine kuhusu malengo yako na vitu unavyotaka kuvifanikisha maishani wengi watakukatisha tamaa. Wanachofikiri au kusema hakijalishi. kila mtu aliyefanikiwa unayemfahamu wewe ana stori nyingi za kukatishwa tamaa alizo kutana nazo pindi anafanya jitihada za kutimiza ndoto yake.

Utakapoitambua ndoto yako na kuamua kuifuata utafungua uwezo mkubwa uliomo ndani yako ambao kukupata kuuona kabla. Utashangaa nguvu kubwa ikikusukuma na kukuongoza.

Unaifahamu ndoto yako? unayajua malengo yako maishani?

 Jaribu kuyatafakari maswali haya, yape utulivu wa kutosha na tafakari ya kina. Jibu unaweza kulipata papo hapo au likachukua muda, labda siku mbili, wiki, mwezi au mwezi kulingana na uzito utakayoyapa.

Jibu maswali haya;

  • Kusingekuwa na kushindwa katika maisha, yaani tungekuwa tunafanikiwa tu kwa kila tunachokifanya, ungechagua kufanya nini au kuwa nani katika maisha yako?
  •  Ungepewa uwezo wa kimiujiza  kubadilisha kitu kimoja hapa duniani papo kwa papo, kingekuwa ni kitu gani? Ungebadilisha nini?
  • Fikiria kuwa umefanikiwa kifedha na huna haja ya kufanya kazi tena, huna haja ya kuwaza tena kuhusu pesa na una muda mwingi wa kufanya unachotaka. Je, ungetumia siku zako kufanya nini?
Kila la heri katika safari ya kutimiza ndoto zako!

0 comments:

Chapisha Maoni