Safari ya
kufikia Mafanikio, katika malengo yoyote uliyojiwekea inaweza kuchukua muda
mrefu au mfupi kulingana na ulivyojipanga na hatua unaochukua.
Hatua zifuatazo zitakusaidia kufanikisha
malengo utakayojiwekea kwa mwaka ujao wa 2015 kwa haraka zaidi.
1.UFASAHA WA LENGO
Ni lazima
ufahamu matokeo ya kile unachotaka kufanya, nikimaanisha kuwa ni lazima uwe na picha halisi ya kile
unachotaka kukifanikisha. Lazima ujue unataka nini au unataka kuwa nani.
Lengo lazima
liwe wazi, lijulikane kabla hujaanza kuchukua hatua yoyote. Kwa maana nyingine
huwezi kuanzisha safari pasipo kujua mwisho wa safari yako.
Unapokuwa na
lengo mahususi ni rahisi kupanga mikakati ya kulifanikisha. Akili na mawazo
huanza kuvutia vitu ambavyo vitarahisisha ufanikishaji wa lengo lako. Ni vema
kujikita hasa kwa kile unachohitaji na kuachana na yale usiyoyahitaji. Kuielekeza akili yako kwenye mambo
usiyoyataka utavutia fikra hasi na kukosa hamasa na msukumo wa kuchukua hatua zaidi za kuelekea kwenye malengo
yako.
2. CHUKUA
UAMUzI
THABITI
Baada ya
kugundua lengo mahususi ni wakati wa kuchukua uamuzi mathubuti wa kufikia
Malengo yako. Ni wakati wa kuamua kuwa unaenda kufanya kile unachotaka kufanya
kwa moyo wako wote, nguvu zako zote na akili yako yote na kwamba ni lazima
ufanikiwe kwa vyovyote vile. Uamuzi huu lazima uwe umetoka moyoni mwako na si
shinikizo au ushawishi wa watu wengine.
Uamuzi
thabiti unadhihirisha kuwa kitu ulichoamua kufanya unakipenda na kimo katika
damu yako. Kwa kufanya kitu ambacho ni shauku ya moyo wako ni rahisi kwako kuzigeuza
changamoto utakazokutana
nazo kuwa fursa zitakazokurahisishia safari ya
kuyafikia Malengo yako. Hautoweza kukata tamaa kwa urahisi hata pale mambo
yanapoonyesha kuwa magumu.
3.CHUKUA WAJIBU BINAFSI
Tambua
kwamba uamuzi uliouchukua ni wako binafsi kwa hiyo uwe tayari kuyapokea mambo
yote ya sasa na yajayo yatakayotokana na uamuzi uliouchukua. Upo tayari kubeba
lawama au pongezi. Hakuna mtu ambaye utamlaumu kwa lolote litakalotokea, hakuna
wa kumsingizia wala kumyooshea kidole. Changamoto zote utazitatua mwenyewe na
utakapoanguka utasimama mwenyewe. Kwa maana nyingine, usitegemee sana msaada
watu wengine.
4. JIAMINI
Kujiamini
kunakuweka karibu na Malengo yako. Woga unakuweka mbali na Malengo yako.
Kujiamini ni nyenzo kubwa katika kufanikisha Malengo yako. Kujiamini ni
kushinda vita kabla ya pambano. Jiamini
na unachokifanya na utazipenda hatua zote unazochukua kuyafikia Malengo yako.
5. UNGANA KIHISIA NA KILE UNACHOTAKA KUFANIKISHA.
Vuta picha
mbalimbali za kihisia kwa lengo unalotaka kulifanikisha na ujione kana kwamba
tayari umeshafanikiwa. Kama hamu yako ni kuwa daktari jione kwamba umeshakuwa
daktari jione kuwa uko katika chumba cha daktari unawahudumia wagonjwa wako kwa
furaha na wao wanafurahia huduma yako. Kama unapenda kuwa mfanyabiashara mkubwa
vuta picha kihisia ukijiona upo na wateja unawahudumia au una saini hundi ama
unaadaa manunuzi ya bidhaa. Kwa kufanya hivi unaihadaa akili yako fichika (subconscious mind) ambayo haijui kutofautisha
kati ya jambo halisi na lisilohalisi hivyo itakuweka katika mazingira
yanayoendana na picha unayoijenga akilini na kuvutia mambo ambayo
yatakurahisishia kufanikisha malengo yako.
6.TAMBUA CHA KUFANYA KUKUFIKISHA KATIKA MALENGO YAKO
Lazima ujuwe
ni nini cha kufanya kukufikisha katika malengo yako. Kwa lugha nyingine ni
hatua gani uchukue ili kufikia malengo yako.
7. JIWEKEE
MPANGO KAzI
Mpango kazi
unahusisha kulivunja lengo kuu katika malengo madogomadogo ili kuweka urahisi
wa kufanikisha adhma yako. Hii ni pamoja na kujipangia muda maalumu wa
kufanikisha lengo lako, na kupanga mikakati itakayokusaidia. Bila kuwa na mpango kazi uliojiandalia wewe
mwenyewe unajipunguzia uwezekano wa kuyafikia malengo yako kwa muda na wakati
unaotakiwa. Pia kuna uwezekano wa kuhama kabisa kwenye lengo na kujikuta unaelekea
kwenye lengo jingine kabisa ambalo hukulitegemea. Zaidi ya hayo, unapojiandalia
mpango kazi unajipa hamasa binafsi ya kuwekeza akili, mawazo na nguvu zaidi
katika malengo yako.
Ni muhimu
kuwa na mpango kazi zaidi
ya mmoja yenye mikakati tofauti ili
usipoteze mwelekeo pale mpango mkuu unapofeli. (mfano Plan A, Plan B, Plan C, nk).
8. CHUKUA HATUA
Baada ya
kujua nini cha kufanya, na kujiandalia mpango kazi, anza mara moja kuchukua hatua, hakuna haja ya kusubiri kila kitu kiwe
tayari. Kumbuka, safari ya maili elfu moja huanza na hatua moja. Anza na
ulichonacho hata kama hakijatimia na utaona hatua nyingine zinajiongeza zenyewe.
Utaanza kuona njia inafunguka na kukuonyesha mwelekeo. Chukua hatua sasa! Bila
kuchukua hatua yoyote itakuwa vigumu kufikia Malengo yako. Kumbuka kuwa pamoja
na kuwa na mipango, mikakati na malengo mazuri, bila kuchukua hatua madhubuti hakuna kitakachoemdelea.
9.JITATHMINI
Je, hatua
ulizochukua zinakupeleka karibu na Malengo yako au nje ya Malengo. Kama hatua
unazochukua zinakuelekeza katika kufanikisha Malengo yako, basi endelea
kuchukua na kuboresha hatua hizo. Lakini kama hatua unazochukua zinakupeleka
nje ya Malengo yako jibu siyo kubadili Malengo……
Jibu ni……..
10. BADILI MIKAKATI
Badili
mikakati na hatua unazochukua kuelekea katika malengo yako.
Na kama bado
haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Badili
mikakati na hatua unazochukua.
Na kama bado
haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Tumia Plan B.
Na kama bado
haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Tumia Plan
C.
Na kama bado
haikupelekei kuyafikia Malengo yako……….
Endelea
kubadili mikakati yako, Mpaka utakapofanikiwa.
Hakuna
kukata tamaa, hakuna kurudi nyuma.
Kila la
kheri.